Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji MpondaNAIBU Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, jana alilazimika kujifungia ofisini na kuzima simu yake kukwepa kuonana na waandishi wa habari ambao juzi aliahidi kuonana nao ili kutoa tamko lake la shinikizo la kutakiwa kujiuzulu.
Mbali na Nkya kujifungia, Waziri wake, Dk. Haji Mponda, naye alifuata nyayo na kugoma kabisa kuzungumzia hatima yake ya uwaziri.
Tanzania Daima ambayo ilifika wizarani hapo majira ya saa 4:00 asubuhi lilishuhudia Dk. Mponda na naibu wake Dk. Nkya wakikataa kuonana na waandishi wa habari waliofika kwa ajili ya kupata maelezo yao.
Dk. Hadji Mponda alisema waziwazi kwamba hana la kuongea pindi waandishi walipotaka kuingia ofisini kwake pamoja na balozi wa Misri ambaye alikuwa amekwenda kumtembelea kwa wakati huo.
Lakini kwa upande wa Dk. Nkya ambaye juzi alionyesha ushirikiano mkubwa na gazeti hili, alikosa ujasiri wa kutoa kauli kama alivyoahidi , huku katibu wake akidai kuwa yuko kwenye kikao.
Majira ya saa saba mchana Msemaji wa Wizara hiyo, Nsychris Mwamaja, alijitokeza na kuwaeleza waandishi wa habari kwamba mawaziri hao katu hawawezi kuzungumza kwa kuwa suala hilo haliko tena ndani ya wizara hiyo.
Juzi Dk. Nkya alisema kuwa jana angetoa kauli na msimamo wake juu ya shinikizo la madaktari la kumtaka ajiuzulu.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment