MKULIMA wa kijiji cha Kibwigwa kata ya Mwayaya wilayani Kasulu, Gaudence Kibiriti, ameuawa na wananchi wa kijiji hicho kwa kunyweshwa tindikali aina ya Caustic.
Wananchi hao walifanya mauaji hayo mwanzoni mwa wiki hii wakimtuhumu kumkingia kifua baba yake, anayetuhumiwa kufanya vitendo vya kishirikina.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana, kwamba baada ya kumwua mkulima huyo, wananchi hao walimshambulia baba yake mzazi, Kibiriti Shingwa, na kumjeruhi kwa kummwagia tindikali hiyo pia.
Alisema awali wananchi hao walivamia nyumbani kwa Gaudence na kurusha mawe juu ya paa la nyumba yake.
Baada ya hali hiyo, Gaudence alitoka nje ili kunusuru maisha yake, ndipo wananchi walipomkamata na kumnywesha tindikali hiyo na nyingine kummwagia mwilini na kumsababishia kifo hicho.
Katika tafrani hiyo kwa mujibu wa Kamanda Kashai, wanakijiji hao walivamia shamba la migomba la marehemu lenye ukubwa wa robo heka na kufyeka mazao yote.
Pia waliharibu nyumba zake mbili na kumjeruhi Shingwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kummwagia tindikali.
Alisema majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Heri katika tarafa ya Manyovu, Kasulu kwa matibabu na juhudi za Polisi kuwatafuta watuhumiwa zinaendelea na hadi jana hakuna mtu ambaye alishakamatwa.
Chanzo: Gazeti la HabariLEO
No comments:
Post a Comment