Tuesday, August 9, 2011

Wabunge wachachamaa, wataka Serikali ioneshe ipo

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amewataka wafanyabiashara wa mafuta wawauzie wananchi mafuta, wakiendelea kugoma hadi saa 12 jioni leo wanyang’anywe leseni.


Zitto, amesema bungeni kuwa, mgomo wa wafanyabiashara ya mafuta haukubaliki na hauvumiliki.


Amesema, wafanyabiashara hao wakendelea na mgomo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likavifungue vituo vya kuuzia mafuta ili wananchi wapate nishati hiyo.


Zitto amesema, ni lazima ionekane kuna Serikali, kuna dola na sheria zinatekelezwa. Ametoa msimamo huo wakati akichangia mjadala wa dharura kuhusu hali mbaya ya upatikanaji wa mafuta nchini.


Amesema, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inapaswa kuwaagiza wafanyabishara wa mafuta kwamba leo lazima wauze nishati hiyo kwa wananchi.


“Ni lazima ionekane kuna Serikali, ni lazima ionekane kuna dola, ni lazima kuwepo usimamizi wa vyombo vya Serikali” amesema.


Amesema, wafanyabiashara wa mafuta wanaonesha ubabe na jeuri ya fedha hivyo Serikali ichukue hatua na kwamba, hana maneno matamu ya kuwaeleza wafanyabiashara.


Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika amesema, Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuchukua hatua kumaliza tatizo la lafuta.


Amelieleza Bunge kuwa, ana ushahidi kwamba, baadhi ya maofisa wa Serikali wanahusika katika suala hilo kwa kuwa wamehongwa.



Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela, amesema, wafanyabiashara wa mafuta wasidhani kwamba wapo juu ya sheria na wanapaswa kuiheshimu Serikali. Mbunge huyo amesema, Ewura na Serikali wanapaswa kuonesha meno.



Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), ameunga mkono kauli ya Zitto kwamba, wafanyabiashara wakiendelea kugoma kuuza mafuta, JWTZ iingilie kati. Mnyaa amesema, Bunge limeshindwa kuisimamia Serikali.

Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama, amesema, Serikali isipochukua hatua kumaliza tatizo la mafuta, haitaheshimiwa.

No comments:

Post a Comment