Wednesday, July 6, 2011

Kupendwa raha, kutendwa matokeo

Niambie mtu wangu, mpango mzima vipi, mambo yanakwenda au ndiyo bado unaungaunga.


Waungwana wana jipya gani hapo, wape hi kwa saana, wakumbushe kwamba starehe gharama, pombe nomaa, na wanapojiramba wamkumbuke kunguru, Tanzania bila Ukimwi inawezekana.

Namshukuru Mungu kwa kile nilichonacho na ninachokipata, amani iwe kwenu, nawapa pole wagonjwa wote na wenye shida mbalimbali za kimaisha ikiwa ni pamoja na waliotendwa au kuachika katika umri mdogo, ndiyo ukubwa huo.

Kama wewe ni miongoni mwa waliotendwa omba Mungu akupe uvumilivu, najua inauma sana, lakini kumbuka kwamba, kupenda raha, kupendwa faraja, kutendwa matokeo.


Ni vigumu kutenganisha maisha ya mwanadamu na mapenzi, sehemu kubwa ya maisha yetu imetawaliwa na mapenzi.


Nimewahi kusikia kwamba, asilimia 70 ya maisha ya mwanadamu huhusiana na mapenzi na pengine ndiyo maana migogoro mingi katika jamii inasababishwa aidha na mapenzi au pesa.

Watu wengi wakiwemo vijana wana migogoro na familia zao, rafiki zao, jirani zao, na hata wafanyakazi wenzao kwa sababu ya mapenzi, na wengine wamepoteza maisha kwa kuwa walipenda au kupendwa.

Kuna wakati huwa najiuliza, maisha yangekuwaje bila mapenzi? Mapenzi ni kitu gani? Kwa nini ujidhuru au kumdhuru mwanadamu mwingine kwa sababu ya mapenzi? Kwani maisha bila mapenzi haiwezekani?

Vijana wengi hawana amani na wengine wapo magerezani kwa sababu ya mapenzi.


Kwa mtazamo wangu walioua au kujiua kwa sababu ya mapenzi hawakuzitendea haki nafsi zao, hawakutumia busara na kujipa muda wa kutafakari athari za uamuzi wao.

Kupenda kupo, lakini uhai na amani ni muhimu zaidi, kujiua si suluhisho la matatizo yetu yakiwamo ya mapenzi.


Kwa nini ufupishe uhai wako kwa sababu ya mwanadamu mwingine? Kwani bila yeye huwezi huishi? Kuachana naye ni mwisho wa kupenda au kupendwa?

Kujiua au kuua kwa sababu ya mapenzi ni ujinga, katika mazingira ya kawaida huyo anayesababisha uue au ujiue mmekutana ukubwani na kama msingefahamiana yupo mwingine ambaye angekuwa na hiyo nafasi uliyompa.

Kuna wanaosema eti watu wanajiua kwa sababu ya hasira, lakini wanasahau kuwa hasira hasara, ipo bora, kukubali matokeo au kuongeza tatizo juu ya tatizo?

Kama una mpenzi, mmeshindwana na imebidi muachane kubali yaishe, chapa mwendo, raha jipe mwenyewe, endelea na maisha yako, usiharibu ndoto zako kwa mambo yanayoweza kuzuilika.


Kama uliweza kuwa naye kwa nini ushindwe kuwa na mwingine? Inahuu?

No comments:

Post a Comment