Sunday, July 24, 2011

Buriani Danny Mwakiteleko

ALIYEKUWA Mhariri Mkuu wa Gazeti la Rai, Danny Mwakiteleko (45) amefariki dunia.


Mwakiteleko pia alikuwa Mhariri Mtendaji Msaidizi wa kampuni ya New Habari Corporation Limited, ya Dar es Salaam.


Aliaga dunia jana alfajiri katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Dar es Salaam, anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Rugombo, Mwakaleli mkoani Mbeya.


Mwili wa marehemu utaagwa nyumbani kwake Tabata, Chang’ombe, kesho Jumatatu na utasafirishwa, atazikwa Jumanne.


Mwakiteleko alipata ajali ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Nadia, lililopamia tela la lori katika Barabara ya Nelson Mandela, Dar es salaam usiku wa kuamkia Jumatano.


Wasamaria wema walimkimbiza Hospitali ya Amana, baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili.


Kwa mujibu wa madaktari, Mwakiteleko alipata majeraha makubwa kwenye paji la uso, Jumatano alifanyiwa upasuaji na kuendelea kuwa katika hali ya kukosa fahamu katika chumba cha Wagonjwa wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).


Rais Jakaya Kikwete alikuwa mmoja wa watu waliofika kumjulia hali juzi hospitalini hapo.


Mwakiteleko alizaliwa Novemba 1966 Rugombo, alipata elimu yake ya msingi Tunduma, kabla ya kujiunga na sekondari ya Iyunga, Mbeya na kisha sekondari ya juu Mzumbe mkoani Morogoro.


Alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwaka 1988 Operesheni Miaka 25, kwa mujibu wa sheria na kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Baada ya kuhitimu mafunzo yake ya Chuo Kikuu mwaka 1993, alijiunga na gazeti la Tanganyika Leo akiwa mwandishi wa habari ambalo alikaa nalo kwa muda kabla ya kujiunga na Habari Corporation na kisha kuhamia Business Times Limited (BTL). Aidha alikuwa ni mmoja wa waasisi wa kampuni ya Mwananchi Communications ambao ni wachapishaji wa gazeti la Mwananchi ambako alifanya kazi kwa miaka saba.


Wakati akifanya kazi Mwananchi alihamishiwa kwa muda Nation Group ya Kenya ambako alifanya kazi hadi yalipotokea machafuko baada ya uchaguzi mwaka 2008.


Aliporejea nchini alijiunga na New Habari Corporation, akiwa Mhariri wa Mtanzania na kisha wa Rai hadi mauti yanamkuta.


Mwakiteleko ameacha mjane, Winifrida na watoto Caro (13) na Vanessa (11). Mungu ailaze roho ya Mwakiteleko mahala pema peponi, Amina.

No comments:

Post a Comment