Friday, June 24, 2011

Zitto ngangari, mawaziri ngunguri

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (katikati), akizungumza na mawaziri nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma. Kutoka kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (Chadema) jana alichafua hali ya hewa bungeni mjini Dodoma baada ya kutoa kulituhumu Baraza la Mawaziri kuwa linatumiwa.


Kauli ya Mbunge huyo machachari ilizua mvutano mkubwa kati yake na mawaziri wa Serikali ya Tanzania.


Zitto aliwatuhumu viongozi hao wa Serikali kuwa wameshawishiwa na watu kulifuta Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) kwa faida ya wachache.


Spika wa Bunge, Anne Makinda amempa siku 7 athibitishe tuhuma hizo. Zitto ni kiongozi wa Chadema, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.


Zitto alitoa tuhuma hizo wakati anachangia azimio la Serikali la kuongeza muda wa uhai wa shirika la hilo.


Zitto alirudia mara tatu kauli hiyo na kuwataka wabunge wasikubali kupitisha azimio hilo kwa kuwa ni 'wizi kwa rasilmali za taifa'.


"Hoja ya kuliongezea muda CHC wa miaka mitatu na baada ya hapo lifutwe na kazi zake apewe Msajili wa Hazina (TR) sio bure, baraza la mawaziri limeshawishiwa ili watu fulani wanufaike," alisema Zitto.


"Mapendekezo hayo yaliletwa kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na kwenye Kamati ya Fedha na Uchumi na zote ziliyakataa... Tukasema CHC iongezewe muda zaidi ili ifuatilie madeni na mali za mashirika kadhaa ambayo zimeonekana kuliwa.


"Ukitaka kuifuta leo, Mheshimiwa Spika, madeni ya mashirika ya umma yatapotea na naamini kuna watu wanafurahia jambo hilo kwani watanufaika. Tumewaagiza CHC wafuatilie madeni hayo, halafu hata kabla hawajaanza kazi, tunasema tunataka kulifuta baada ya miaka mitatu, siyo sahihi CHC ni jicho letu la kufuatilia ubadhirifu katika mashirika ya umma."


"TR (Msajili wa Hazina) ana majukumu mengi na tayari tumeona ameshindwa kufuatilia mashirika mengi. Kuna mashirika 25 na taasisi zingine kadhaa hana hati ya mashirika hayo wala hajui mali. Unawezaje kumwongezea majukumu kama huo siyo mpango wa watu kutaka kutuhujumu?"


"Naombeni waheshimiwa wabunge kwa umoja wetu, bila kujali tofauti za itikadi zetu, tulikatae azimio hili, limeletwa baada ya mawaziri kupitiwa na ma-lobbyist(washawishi). Halina manufaa kwa taifa, ni wizi na uporaji wa mali ya umma.


Tuliliagiza shirika hilo lisaidie kufuatilia ubadhirifu kwenye mashirika ya umma, sasa leo tunataka kuiondoe hope (matumaini )yote kwa azimio hilo! Tusikubali,"


Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kapteni George Mkuchika alisimama na kuomba mwongozo wa Spika.


"Mheshimiwa Spika, natumia kanuni inayozuia mbunge kutoa maneno ya kuudhi na lugha chafu bungeni."Mimi ni mjumbe wa baraza la Mawaziri, sijafikiwa na mtu na pia naamini hakuna mmoja wetu aliyepitiwa. Mheshimiwa Zitto umetudhalilisha wabunge wenzio. Spika naomba mwongo wako."Spika Anne Makinda akasema, "Waheshimiwa wabunge, kwa kuwa azimio hilo limekuja kwa dharura, naomba kwanza tusiingize mambo ambayo yatachelewesha utekelezaji wake. CHC inatakiwa kufa ifikapo Juni 30, sasa leo tupitishe kwanza muda huo ulioombwa halafu mijadala mingine iendelee baadaye. Mheshimiwa Zitto endelea.


"Zitto akaendelea, "Nasisitiza kwamba baraza la mawaziri limepitiwa na kufanyiwa lobbying (ushawishi). Ila, ninachosema ni wabunge kuwa makini na kutokubali kupitisha azimio hili kwa kuwa tunawapa ulaji watu.


Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliomba tena mwongozo wa Spika.


"Nasikitika kusema kuwa hata baada ya wewe mheshimiwa Spika kutoa mwongozo katika suala hilo, yeye (Zitto) ameendelea kurudia, maana yake kwamba ana hakika na kile anachokisema. Sasa, naomba atoe ushahidi.


Spika alionekana kutojali ombi la Lukuvi, akamtaka Zitto aendelee kutoa hoja yake, Zitto akaendelea


"Napenda kurejea kwamba, maamuzi haya ni ushawishi wa lobbyists, Kama sivyo, serikali ilete hapo mbele pendekezo la kamati lililoitaka liipe miaka mitatu shirika hilo na baadaye lifutwe na kazi zake zichukuliwe na TR. Tusiruhusu baraza la mawaziri kuendeshwa na lobbyists"


Lukuvi aliomba tena mwongozo wa Spika akimtaka Zitto atoe ushahidi.


"Cabinet (Baraza la mawaziri), kamati za Bunge kazi yake ni kuishauri baraza la mawaziri na ushauri huo siyo lazima usikilizwe.""Cabinet (Baraza) halifanyi kazi kwa shinikizo la mtu. Sasa, tunamtaka mheshimiwa Zitto aseme ni kina nani waliorubuniwa katika cabinet, na wamerubuniwa na nani? Baraza la mawaziri ni kikao huru ambacho hakina uhusiano wowote na watu wengine."


Lukuvi alipomaliza kuzungumza alisimama, Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki- Chadema) na kuomba mwongozo wa spika akisema, "Mheshimiwa Spika, Kanuni ya 63 (3 )na (4) inaeleza kuwa mtu wa kwanza mwenye wajibu wa kuthibitisha hilo ni serikali. Lukuvi athibitishe kwa kiwango cha kuliridhisha bunge na baadaye Zitto ajitetee."


Spika Makinda alisimama akasema,"Nyie watu mnapenda sana kubadilisha mambo. Baraza la mawaziri haliwajibiki kwa Bunge. Anayetakiwa kuthibitisha hapo ni Zitto na sasa namtaka alete uthibitisho huo, Juni 29 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment