RAIS Jakaya Kikwete amesema, umasikini nchini si laana ya Mungu, watanzania wakitumia maarifa hasa katika kilimo watajikomboa na nchi itapaa kuwa taifa tajiri.
Dk Kikwete amesema, mabadiliko yanawezekana, mageuzi ya kilimo hayawezi kusubiri zaidi, na huu si wakati wa kutunga maazimio mapya bali vitendo.
Rais Kikwete ameyasema hayo wakati anazindua azimio la Kilimo kwanza, sanjari na kufungua rasmi maonyesho ya kilimo ya Nane Nane kitaifa katika uwanja wa Nzuguni, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
“Kuna vitu tukivifanya hali yetu ya maisha inabadilika…jamani mabadiliko yanawezekana” amesema Dk Kikwete na kuwataka watanzania wafanye kazi badala ya kukaa vijiweni kusubiri maisha bora.
“Maana sio ukae kijiweni ukingoja kilimo kitakufanyia nini” amesema na kuwaeleza wavivu kwamba, kamwe hawatapata maisha bora.
Amewataka watanzania waache kutumia muda wa kazi kuzurura au kucheza ngoma, na pia wabadili fikra zao.
Amesema, watanzania wanapaswa kudhamiria kuacha kilimo cha kizamani, wajitume, na wawe wabunifu katika uzalishaji na fani nyingine, na kwamba, lazima wakulima Tanzania waache kutumia jembe la mkono,
watumie majembe yanayokokotwa na wanyama kazi au matrekta.
watumie majembe yanayokokotwa na wanyama kazi au matrekta.
“Kilimo ndiyo moyo wa maendeleo ya nchi yetu, kilimo ndiyo kila kitu” amesema Rais katika ufunguzi huo uliohudhuriwa pia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baadhi ya mawaziri, wabunge, watendaji wa Wizara mbalimbali, na wananchi.
“Mapinduzi ya kilimo ndugu zangu yanawezekana na yatafanikiwa kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake” amesema Rais na kubainisha kwamba, kuna kazi kuifafanua vizuri dhana ya kilimo kwanza wananchi
waielewe.
Rais Kikwete amesema, Kilimo Kwanza si mbadala wa Mkakati wa Taifa wa kukuza Uchumi na Kupunguza umasikini (MKUKUTA) na kwamba, dhana hiyo haipingani na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2000-2025.
Amesema, Mpango wa Taifa wa Kuboresha Sekta ya Kilimo (ASDP) utatekelezwa kwa kuzingatia azimio la Kilimo Kwanza. “Hakuna lugha gongana wala hakuna kitendo gongana” amesema.
Amesema, lengo kubwa la azimio la Kilimo Kwanza ni kuwawezesha wakulima wadogo na wakubwa waingie kwenye kilimo cha kisasa na cha kibiashara. Dk Kikwete amesema, ushiriki wa sekta binafsi ni lazima katika kutekeleza azimio la Kilimo Kwanza.
No comments:
Post a Comment