Friday, October 31, 2014

Ajira maofisa Ustawi wa Jamii


OFISI ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imewataka wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, manispaa na majiji kutoa nafasi za ajira za maofisa Ustawi wa Jamii na Lishe ili  kusimamia  utoaji wa elimu ya afya ya jamii.



Mbali na kuelekezwa kutoa nafasi hizo, pia wametakiwa kuandaa miongozo na kutenga  bajeti na kuiingiza katika makadirio ya bajeti, zinazoandaliwa hivi sasa za halmashauri ili kazi za maofisa wa Ustawi  wa Jamii na wale wa Lishe watakapoajiriwa waanze kazi zao mara moja.




Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi (Afya), Dk Deo Mtasiwa,  alisema Serikali imekuwa ikitoa vibali vya ajira katika idara mbalimbali za Serikali, ikiwemo  kwa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji kuomba kibali cha kuajiri wataalamu wa sekta mbalimbali za serikali.



Alisema hayo katika  hotuba yake ya ufungaji wa mkutano mkuu wa 34 wa Chama cha Wanataaluma wa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO), uliochukua siku tatu mjini Morogoro.



Dk Mtasiwa alisema kwa mwaka huu Ofisi ya Waziri Mkuu,Tamisemi, imetoa maagizo na kuzielekeza halmashauri kutoa nafasi za ajira kwa Maofisa Ustawi wa Jamii pamoja na Lishe ili waweze kufanya kazi kimuundo na mfumo wa kiserikali katika utoaji wa huduma za wananchi hadi ngazi za vijiji.

HABARILEO, Oktoba 31, 2014

No comments:

Post a Comment