Mbunge
wa jimbo la Ubungo, John Mnyika akichangia mjadala wa bajeti bungeni
mjini Dodoma kabla ya kutolewa nje ya ukumbi huo na Naibu Spika, Job
Ndugai.
Mbunge
wa jimbo la Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) akitoka ndani ya ukumbi wa
bunge, mara baada ya Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kumuamuru atoke kwa kuwa alikataa kutii amri ya kumtaka kufuta kauli.
Mbunge wa jimbo la Ubungo, John Mnyika akitoka katika
ukumbi wa Bunge
la Tanzania mjini Dodoma baada ya kukataa kufuta kauli iliyodaiwa
kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa dhaifu.
Askari wa Bunge akimuongoza Mh. John Mnyika.
Askari
wa Bunge wakihakikisha Mbunge wa Ubungo Mh. John Mnyika akiondoka
katika eneo la viwanja vya Bunge baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kumtoa
nje ya ukumbi wa Bunge.
John Mnyika akiongea na Waandishi wa Habari baada ya kutoka nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Askari
Polisi wa Bunge, wakimwamru Mbunge wa jimbo la Ubungo, John Mnyika
(Chadema), kuondoka maeneo ya bunge, baada ya kutolewa nje na Naibu
Spika, Job Ndugai kutokana na kukataa kuondoa hoja yake
Askari Polisi wa bunge walilisindikiza gari lililombeba mbunge wa Ubungo, John Mnyika mara baada ya kutolewa nje na Naibu Spika, Job Ndugai
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo wakati akichangia Bajeti ya serikali ya
mwaka 2012/13 katika mkutano unaoendelea.
Mnyika alisema, bajeti iliyowasilishwa
bungeni haitekelezi ilani ya CCM wala mpango wa maendeleo wa miaka
mitano ambao wabunge walipitisha.
Mnyika alisema umaskini wa Mtanzania na kilio cha maji nchi nzima
kimetokana na udhaifu wa rais wa nchi, upuuzi wa CCM na uzembe wa
wabunge.
“Ubovu wa bajeti hii ni matokeo ya udhaifu wa Rais Kikwete, yeye ndiye
aliyesaini Mpango wa Taifa wa miaka mitano kama Kiongozi Mkuu wa nchi
tena kwa wino mwekundu kama Amiri Jeshi Mkuu.
“Na yeye ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri, bajeti hii iliyoacha
kuzingatia Mpango wa Taifa imepita kwenye baraza aliloliongoza, pia
kushindwa kutekelezwa kwa bajeti iliyopita ni matokeo pia ya udhaifu wa
taasisi ya urais.
“Kwa mujibu wa Katiba rais ndiye ambaye anapeleka
bajeti bungeni, waziri mwenye dhamana anapeleka tu kwa niaba. Rais
amepewa mamlaka makubwa juu ya bajeti, ibara ya 99 imeweka mipaka kuhusu
mambo ambayo Bunge lina mamlaka nayo huku ibara ya 90 inasema Bunge
likiikataa bajeti, rais ana mamlaka ya kuvunja Bunge.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
William Lukuvi, alitoa utaratibu na kudai kwa mujibu wa kanuni za Bunge
namba 61 Mnyika alitumia maneno ya kuudhi kwa kumwita Rais Kikwete kwa
kumtaja jina kuwa ni dhaifu na kusema CCM ni upuuzi.
“Nataka niseme kuwa katika watu ambao nawaheshimu ni Mheshimiwa
Mnyika, tena nasema kutoka moyoni lakini kwa hili mdogo wangu umepotoka,
kwa mujibu wa kanuni mbunge yeyote haruhusiwi kumtaja mtu yeyote ambaye
hayumo humu ndani ya Bunge, maana hawezi kupata nafasi ya kujitetea,
hivyo ni vema ukafuta kauli hiyo,” alisema Lukuvi.
Naibu Spika Job Ndugai alikubaliana na hoja ya Lukuvi ya kumtaka Mnyika kufuta kauli yake lakini Mnyika hakuwa tayari kufuta kauli yake ya kumwita Rais
Kikwete dhaifu, hata alipoombwa tena kufanya hivyo na naibu spika.
Kutokana na hali hiyo, Ndugai alitumia kanuni ya 73 (2) (3) ya kumtaka mbunge huyo atoke nje.
“Sasa ndugu wabunge humu ndani tunaendeshwa kwa kanuni na kwa kuwa
mimi ni Naibu Spika wa uhakika sasa ni lazima nihakikishe sheria
zinafuatwa.
“Kutokana na kanuni ya 73 kifungu cha 2 na 3, kifungu cha 2 kinaeleza
mbunge yeyote haruhusiwi kutumia lugha ya kuudhi wala matusi na mbunge
akifanya hivyo anatakiwa kufuta kauli yake kwa maelekezo ya Spika kwa
kutumia kanuni zilizopo na endapo mbunge huyo atashindwa kufuta kauli
hiyo anatakiwa kutolewa nje hadi muda wa shughuli za Bunge uliobaki
uishe.
“Kifungu cha tatu kinaelekeza kuwa Mbunge ambaye atatakiwa na Spika
kutoa uthibitisho kwa jambo ambalo alilisema bungeni na kushindwa
kufanya hivyo anaweza kufutiwa vikao vitano mfululizo vya Bunge, sasa
kifungu cha 3 nakiacha kutokana na Mheshimiwa Mnyika kushindwa kufuta
kauli yake, sasa nawaagiza askari wangu waliopo hapa ndani kumtoa John
Mnyika nje ya ukumbi wa Bunge,” alisema Ndugai.
No comments:
Post a Comment