Bodi
ya Wakurugenzi na wafanyakazi wa Jambo Concepts Ltd inayochapisha
gazeti la Jambo Leo na Jarida la Jambo Brand wanapenda kuwajulisha
Watanzania na wanahabari wote nchini kwamba Mhariri Mkuu wa gazeti
hilo, Willy Edward Ogunde amefariki dunia mjini Morogoro.
Tunasikitika mno kuondokewa na
mfanyakazi wetu ambaye alikuwa mchapakazi na mwenye ueledi mkubwa
katika tasnia ya uandishi wa habari. Kwa wanaomfahamu Willy watakuwa
mashahidi wa hilo tunalosema.
Hadi sasa hatujapata taarifa rasmi
za kidaktari kuhusu kifo chake, lakini taarifa zilizopatikana kutoka
kwa ndugu wa marehemu zinasema alikuwa anasumbuliwa na tatizo la moyo.
Mhariri
Mtendaji wa kampuni ya Free Media ambayo inachapisha magazeti ya
Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda akimpa pole Mkurugenzi wa Jambo Concepts,
Juma Pinto kufuatia kifo cha Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo, Willy
Edward kilichotokea mkoani Morogoro usiku wa kuamkia leo. (Picha zote
na Mpiga Picha wa Habari Mseto Blog).
Mkurugenzi wa Jambo Concepts,
Juma Pinto akilia kwa uchungu baada ya kuona gari lililokuwa limebeba
mwili wa aliyekuwa Mhariri Mkuu wa Jambo Leo marehemu Willy Edward
likiingiza mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhia maiti katika
hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar
Mhariri
wa gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Salehe Mohamed (kushoto), Mhariri
wa Habari Mtanzania, Mwandishi wa Michezo Tanzania Daima, Ruhazi Ruhazi
na Frank Balile wa gazeti la Super Star
Baadhi
ya Wahariri na waandishi waandamizi wakiushusha mwili wa marehemu ili
kuhifadhiwa katika hospitali ya Taifa muhimbili, Dar es Salaam mara baada ya kuwasili
kutoka Morogoro.
Mwili wa marehemu Willy Edward ukiingizwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili. (Picha zote na www.francisdande.blogspot.com)
WASIFU
Willy
Edward Daniel Ogunde ambaye alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo
Leo alizaliwa Machi 7, 1974 katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Alisoma shule ya msingi Mapinduzi
mwaka 1983 hadi 1989 kisha elimu ya Sekondari katika shule ya Serengeti
mwaka 1990 hadi 1993.
Baadaye alijiunga na shule ya Sekondari Musoma
kidato cha tano na sita mwaka 1994 na 1995.
Mwaka 1996 alijiunga na Kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya BTL akiwa mwandishi wa gazeti wakati huo likiitwa Majira Jioni.
Akiwa na kampuni hiyo alipata mafunzo mafupi ya kikazi yakiwemo ya kompyuta na ya uandishi wa habari.
Mwaka 1998 alihamishwa kitendo
kutoka kwenye gazeti la Majira Jioni kwenda kwenye gazeti jipya la Dar
Leo na kuwa mwandishi wa habari wa gazeti hilo lakini pia akishikilia
nafasi ambazo alikuwa akizitumikia kwenye gazeti la Majira Jioni.
Alifanikiwa kuaminika na kutokana
na uwezo wake kazini alipanda daraja na kuwa Mhariri wa gazeti la Dar
Leo kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.
Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007
alikuwa akitumikia nafasi ya Mhariri wa Msaidizi wa Michezo gazeti la
Majira na baadaye 2006 hadi 2007 akawa Mhariri wa Michezo wa gazeti
hilo .
Mwaka 2006 hadi 2007 alipata cheti cha elimu ya uandishi wa habari katika Chuo cha Ceylon (CSJ).
Amesafiri nchi mbalimbali duniani
katika kuripoti habari za michezo na burudani ikiwemo Afrika Kusini
mwaka 2003 hadi 2006 kwenye mashindano ya Big Brother Africa.
Pia mwaka 2007, 2008 na 2009 Kenya, Senegal na Uingereza kuripoti habari za michgezo kupitia Super Sport.
Mei mwaka huu alisafiri kwenda
nchini Uturuki kwenye kongamano la wadau wa masuala ya mawasiliano
ambako alikuwa kiongozi wa wahariri waliotoka Tanzania na kutoa mada
iliyohusu mwenendo wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
Nje ya kazi ya uandishi wa habari
mwaka 2008 na 2009 alifanya kazi katika kampuni ya matangazo ya ZK
akiwa Ofisa Habari na Uhusiano.
Miongoni mwa vyombo vya habari
ambavyo aliwahi kufanya kazi enzi za uhai wake ni pamoja na Kampuni ya
New Habari ambayo aliitumikia mwaka 2007 na 2008 akiwa Mhariri Msaidizi
wa gazeti la Bingwa.
Hatimaye mwaka 2008 alikuwa Mhariri
Mkuu wa gazeti la Bingwa kabla hajaacha kazi katika kampuni hiyo na
kujiunga na Kampuni ya ZK.
Alijiunga na gazeti la Jambo Leo
mwaka 2010 akiwa Mhariri wa Habari na kuanzia mwaka jana hadi mauti
ilipomkuta alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo.
Taarifa hii imetolewa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Jambo Concepts Ltd,
Ramadhan Kibanike
No comments:
Post a Comment