BARAZA la Mitihani la Tanzania, limetangaza matokeo ya kidato cha
sita ambapo yameonyesha kuwa shule ya wasichana ya Marian Girls
inaongoza; ufaulu umeongezeka, wavulana wakiwa vinara, huku shule sita
za serikali zikiwa miongoni mwa shule kumi bora.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo,
Dk. Joyce Ndalichako, alisema kuwa Marian Girls imetoa wasichana watano
waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kwa kombinesheni ya PCM.
Aliwataja wasichana hao kuwa ni Faith Assenga, Imaculate Mosha, Rachel
Sigwejo, Mary Kiangi na Nashivai Kivuyo ambao wameongoza kwa mchepuo wa
masomo ya sayansi kwa kombinesheni ya PCM.
Alisema ufaulu kwa mwaka huu, umeongezeka hadi asilimia 87.58
ikilinganishwa na asilimia 87.24 mwaka jana na wavulana wakiongoza kwa
asilimia 87.69 dhidi ya 87.37 kwa wasichana.
Dk. Ndalichako alisema idadi ya wavulana imeongezeka ikilinganishwa
na wasichana pia kutokana na ubora wa ufaulu, ambapo wasichana 12,151
wamefaulu katika madaraja ya I-III ambayo ni sawa kwa asilimia 79.41
huku wavulana wakiwa ni 22, 849 ikiwa ni sawa na asilimia 79.51.
Alisema wavulana waliopata daraja la kwanza ni 1,717 huku wasichana
wakiwa 782, na daraja la II, wanafunzi wavulana wakiwa 5,878 na
wasichana wakiwa 3,248.
Kwa mujibu wa Ndalichako, licha ya ufaulu wa mwaka huu kupanda, ufaulu
wa masomo ya Chemistry, Basic Applied Mathematics, Economics na General
Studies umeshuka.
Alizitaja shule sita za serikali zilizofanya vizuri katika shule bora
zenye wanafunzi zaidi ya 31 moja kuwa ni pamoja na Kibaha ya mkoa wa
Pwani, Mzumbe (Morogoro), Msalato (Dodoma), Tabora Boys (Tabora) na
Ilboru (Kisimiri).
Shule binafsi iliyoongoza katika kumi bora ni Marian Girls, ikifuatiwa
Feza Boys na St. Mary’s Mazinde juu iliyoshika nafasi ya tisa na shule
ya Consolata Seminary nafasi ya kumi.
Katika mkutano wake na wanahabari, Dk. Ndalichako alitaja shule kumi
ambazo zimeshika nafasi ya mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 30 ambazo ni
Pemba Islamic College na Uweleni za mkoa wa Pemba, Zanzibar Commercial
na Haile Selassie na Laureate International na Mzizini pamoja na Lumumba
za mkoa wa Unguja, Kongwa na Ben Bella za Dodoma pamoja na Mlima Mbeya
High School ya mkoani Mbeya.
“Ubora wa shule umepangwa kwa kutumia kigezo cha ‘Grade Point Average
(GPA)’ ambapo A=1, B=2, C=3, D=4 na E=5 pamoja na S=6 huku F=7, shule
zimegawanyika makundi mawili kulingana na idadi ya watahiniwa 30 na
zaidi ambao jumla yao ni 326 na shule zenye watahiniwa pungufu ya 30
ambao jumla yao ni 139,” alisema.
Katibu mtendaji alisema kuwa watahiniwa waliofanya vizuri zaidi
kitaifa wamepatikana kwa kuangalia GPA kwenye masomo ya kombinesheni
pamoja na alama za jumla walizopata, lakini masomo ya hiyari
hayakujumuishwa katika kupanga wanafunzi bora.
“Mwanafunzi aliyeongoza katika mchepuo wa masomo ya sayansi ni Faith
Assenga wa Marian Girls, akifuatiwa na Zawadi Mdoe wa shule ya Feza
Boys, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Belnadino Mgimba wa shule ya
Minaki na Jamal Juma wa Feza Boys akishika nafasi ya nne na mwanafunzi
wa Marian Girls akishika nafasi ya tano.
Alisema, “Wavulana watano bora kitaifa kwa masomo ya Sayansi ni pamoja
na Zawadi Mdoe wa Feza Boys, Belnadino Mgimba wa Minaki na Jamal Juma
wa Feza Boys na Gwamaka Njobelo na Nockson Mwamsojo kutoka sekondari ya
Mzumbe.”
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment