Thursday, May 17, 2012

Buriani Patrick Mafisango

 Wachezaji Haruna Niyonzima wa Yanga (kushoto) na Uhuru Selemani wa Simba wakiwa na majonzi baada ya kuuona mwili wa Mafisango katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.

Patrick Mutesa mafisango amekufa alfajiri ya leo jijini Dar es Salaam.

Mchezaji huyo 'kiraka', ameaga dunia muda mfupi baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Tazara.

Mafisango alikuwa na uwezo wa kucheza namba 6, 8, 10 na hata 11.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, Mafisango alipata ajali hiyo wakati akiendesha gari, na kwamba, alikuwa anamkwepa mwendesha pikipiki.

Rage amesema, wakati anamkweka mwendesha pikipiki, gari hilo liliingia mtaroni, mchezaji huyo raia wa Rwanda akaumia sana, na aliaga dunia muda mfupi baadaye.

Amesema, Mafisango alikuwa na rafiki yake, na mtu mwingine, na kwamba, wameumia.

Mafisango ameaga dunia siku chache baada ya kocha wa timu ta taifa ya Rwanda kumuita katika timu ya taifa ya nchi hiyo.

  Mbunge wa jimbo la Korogwe CCM Steven Ngonyani Prof Maji  Marefu akizungumza na wanahabari hospitalini hapo kuelezea masikitiko yake kuhusu kifo cha mchezaji huyo.
 Haruna Moshi akitoka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti huku akilia kwa uchungu baada ya kuhakikisha kweli mwenzao Patrick Mafisango ameaga dunia.
 
Mchezaji wa zamani wa Simba Boniface Pawasa akilia kwa uchungu huku akifarijiwa na Mchezaji Uhuru Selemani.
 
Pawasa amesema jana walikuwa naye kwenye muziki katika klabu ya Maisha Oysterbay wakati bendi ya Akudo Impact ikifanya onyesho klabuni hapo na marehemu alimuaga kwamba anaenda nyumbani baadae akapigiwa simu kwa simu ya marehemu akiambiwa mwenye simu hii amefariki dunia kwa ajali.
 

Uongozi wa Simba umesema, unawasiliana na Ubalozi wa Rwanda na mashirika ya ndege ili kukamilisha utaratibu wa vibali mbalimbali tayari kwa kuusafirisha mwili wa marehemu kwenda nchini Rwanda kwa mazishi na taarifa kamili ya lini utasafirishwa itatolewa kesho mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote.

 
 Aliyewahi kuwa mchezaji wa timu ya Simba Mrundi Ramadhana Wasso akihojiwa na waandishi wa habari kuelezea masikitiko yake kutokana na msiba huo.
 
(Picha kwa hisani ya blog ya Fullshangwe).
 

No comments:

Post a Comment