Msichana Imaculata Joseph (19) amesema, amemuuza mtoto wake
mchanga wa kike mwenye umri wa miezi miwili.
Binti huyo mkazi wa eneo la Majengo Mtaa wa Gezaulole mkoani
Mtwara, amewaeleza Polisi kuwa amekiuza
kichanga hicho kwa bei ya milioni 1.5/-, na kwamba, ametumia fedha hizo kununua
pikipiki kwa ajili ya biashara.
Hata hivyo bado kuna utata kuhusu sakata hilo kwa kuwa
msichana huyo anayedaiwa kuwa mlevi wa pombe za kienyeji, pia amesema kuwa amemuuza mwanawe kwa shilingi
lakini mbili.
Utata kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo umezidi kuongezeka kwa
kuwa, inadaiwa kuwa, msichana huyo alikaririwa akisema kilabuni kuwa, anataka
kumuuza mwanawe, na siku chache baadaye, kichanga hicho hakikuonekana tena, na
mama huyo akadai kuwa mwanawe kaibwa.
Ofisa Mtendaji wa eneo analoishi msichana huyo, Yusuf Mfaume
amethibitisha kutoweka kwa kichanga hicho kilichotimiza umri wa miezi miwili
Aprili 25 mwaka huu.
Mfaume amesema, taarifa kuhusu kupotea kwa kichanga hicho
zinachanganya, na kwamba, msichana huyo ni mwenyeji wa kijiji cha Lulindi
wilayani Masasi.
Inadaiwa kuwa, Imaculata amemuuza mwanawe huyo kwa mwanamke
anayetoka Morogoro.
Kwa mujibu wa Mfaume, msichana huyo ni mlevi, na kwamba, hata
yeye alizungumza naye baada ya kumnunulia pombe za kienyeji. Polisi wamemuachia
binti huyo kwa dhamana, uchunguzi unaendelea.
No comments:
Post a Comment