Friday, March 2, 2012

Ni Sioi Vs Nassari Ubunge Arumeru

MBINU za vigogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutaka kumkwamisha Sioi Sumari kuwania ubunge wa Arumeru Mashariki katika uchaguzi mdogo utaofanyika Aprili mosi mwaka huu zimegonga mwamba.


Sioi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari, jana alishinda tena kura za maoni kwa kupata kura 761 huku mpinzani wake William Sarakikya akiambulia kura 361 kati ya kura 1,124.


Mchakato huo wa kurudia kura za maoni uliamriwa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho baada ya wajumbe wake kudai kuwa hakuna mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 kama kanuni za chama hicho zilivyo.


Kabla ya CC kuketi, wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho waligawanyika pande mbili ambapo upande mmoja ulikuwa ukitaka Sioi aondolewe na mwingine ukipinga.


Katika uchaguzi wa awali Sioi aliongoza kwa kupata kura 362 akifuatiwa na Sarakikya aliyepata kura 259, Elirehema Kaaya (205), Elishilia Kaaya (176), Anthony Msani (22) na Rishiankira Urio (11).


Matokeo hayo yalizusha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho kwa madai mgombea huyo si raia wa Tanzania, alitumia rushwa na pia anapigiwa chapuo na kundi la mmoja wa watu wanaodaiwa kutaka kuwania urais mwaka 2015.


Katika kikao cha CC, kilichoongozwa na Rais Jakaya Kikwete iliamriwa kuwa Sioi na Sarakikya washindanishwe tena ili apatikane mgombea atakayepewa baraka za kuipeperusha bendera ya chama katika uchaguzi huo.


Inadaiwa katika kikao hicho makundi hasimu yalitunishiana misuli kwa lengo la kupanga safu za kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa chama utakaofanyika baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015.


Kikao hicho kilimteua Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa, kuwa msimamizi wa zoezi la kura za maoni zilizofanyika jana akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu (bara) John Chiligati.


Akitangaza matokeo hayo jana, Pius Msekwa alisema Sioi Sumari alipata kura 761 na William Sarakikya akiambulia kura 361 kati ya 1,124 zilizopigwa ambapo kura mbili ziliharibika.


Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo Sarakikya alisema ameyakubali huku akimtakia kila la kheri Sioi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa jimbo hilo.


Sioi aliwashukuru wajumbe kwa kuonyesha imani kubwa kwake na kuwaomba waanze kuizungumza vizuri CCM kwa lengo la kuisafishia njia ya kushinda uchaguzi wa Aprili Mosi.


Naye, Msekwa alisema kuwa alitumwa na Kamati Kuu kuangalia hali halisi ya mkutano huo aliyoielezea kuwa ilikuwa ni ya utulivu na kuwapongeza wajumbe hao ambao walikuwa wakishangilia kwa sauti kubwa.


Baada ya kumaliza kuzungumza, wana CCM waliokuwa ukumbini hapo wakishangilia walimbeba juu Sioi na kuondoka naye mpaka kwenye gari lake ambapo walitawanyika kwenye eneo hilo kutokana na hofu iliyotanda kuwepo kundi kubwa la wafanyakazi wa Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru).


Awali kabla ya uchaguzi kuanza Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Chiligati, alisema kuwa wagombea hao hawatajieleza kwani walishafanya hivyo wakati uchaguzi ulipofanyika kwa mara ya kwanza ambapo aliwataka wagombea kusimama kusalimia wajumbe na kisha kuwaomba kura.


Alisema kuwa kamati ya siasa wilaya ilitazamiwa kukaa jana baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa ambapo leo kamati ya siasa mkoa inakaa na kesho Kamati Kuu (CC) inatazamiwa kukaa kujadili na kutangaza jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM Arumeru Mashariki.


Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment