Thursday, March 1, 2012

Mwanamke aliyekutwa na fuvu la binadamu aaga dunia

MWANAMKE Fatuma Kachingo (42), mkazi wa Wami Dakawa katika Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 10 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumiliki fuvu la binadamu, amefariki dunia.

Mfungwa huyo amefariki mwanzoni mwa wiki hii katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro alikolazwa akisumbuliwa na ugonjwa wa uvimbe tumboni hali iliyosababisha afanyiwe upasuaji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo alisema hayo juzi ofisini kwake na kuongeza kuwa Fatuma alihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa baada ya kukiri kosa.

Kamanda huyo alisema, muda mfupi baada ya kufanyiwa upasuaji huo, mwanamke huyo ambaye alikuwa ni mfungwa alifariki dunia.

Alisema utaratibu wa mazishi kwa mujibu wa sheria unafanyika, ambapo kwa sasa mwili huo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Mwanamke huyo alikutwa na fuvu na ngozi ya binadamu pamoja na vifaa vingine vinavyodhaniwa kuwa vya kishirikina akiwa na mumewe Mogela Victory (38).


Vitu vingine walivyokutwa navyo wakati huo ni magamba ya konokono vilivyodhaniwa pia kutumika katika ushirikina.

Mwanamke huyo na mumewe walikamatwa Oktoba 29 mwaka jana eneo la Wami Dakawa, wilayani Mvomero na walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza kusomewa mashitaka yao Novemba mosi mwaka jana.

Hata hivyo watuhumiwa hao walipofikishwa mahakamani kujibu mashitaka, Fatuma alikiri kosa na kuhukumiwa kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu kinyume cha sheria na mumewe alikana mashitaka na kesi yake kupangiwa siku nyingine.


Chanzo: Gazeti la Habarileo

No comments:

Post a Comment