Wednesday, March 7, 2012

Mpinzani wa Chadema Arumeru achukua fomu

MBIO za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki zimefikia patamu baada ya mgombea wa CCM, Siyoi Sumari jana kumalizia hatua ya awali ya wagombea kuchukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwa mbwembwe na shamrashamra za aina yake.


Siyoi alifika katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arumeru Mashariki, jana akiwa mgombea wa sita kuchukua fomu hizo baada ya wenzake watano kutoka vyama vya upinzani, kufanya hivyo juzi.


Wagombea waliochukua fomu hizo juzi na vyama vyao kwenye mabano ni Joshua Nassari (Chadema), Abraham Chipaka (TLP), Shabani Kirita (SAU), Charles Msuya (UPDP), Mohamed Abdallah Mohamed (DP). Mwisho wa kurudisha fomu ni kesho.


Msafara wa Siyoi uliongozwa na maandamano ya pikipiki na magari kadhaa na alifika kwa msimamizi huyo wa uchaguzi akiwa amefuatana na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, Katibu wa CCM Wilaya ya Arumeru, Edson Lihweuli na wafuasi wengine wa chama hicho majira ya saa 5:08 asubuhi.


Siyoi na viongozi wachache waliingia katika Ofisi ya Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru, Trasias Kagenzi huku wafuasi zaidi ya 30 wakitaka kuingia kushuhudia tendo la uchukuaji fomu la mgombea wao lakini walizuiliwa kutokana na ufinyu wa nafasi.


Mara baada ya msimamizi huyo kutoa maelekezo kwa mgombea na kumkabidhi fomu hizo nne, Chatanda aliwataka wanaCCM waliofika kushuhudia tukio hilo kuwa kitu kimoja na kuongeza ushirikiano ili mgombea wao aibuke na ushindi.


“Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wetu kuja kuchukua fomu... ushirikiano huu uendelee ili kukirudishia chama chetu heshima na kutwaa kiti hiki, kwa kuwa mgombea wetu bado ni “Mwali” hataongea mengi leo wasije wakasema huyu mwali vipi?” alisema Chatanda.


Siyoi aliwashukuru kwa kutumia lugha ya Kimeru kisha kuondoka kwa maandamano kuelekea ofisi ya CCM Wilaya eneo la Sekei katika Halmashauri ya Arusha kwa ajili ya kupata wadhamini wasiopungua 25.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment