RAIS wa Chama cha Madaktari Nchini (MAT), Namara Mkopi, ameshikilia msimamo wao wa kugoma kuanzia kesho ikiwa serikali itaendelea kumkumbatia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya.
Dk. Mkopi amesema, katika kikao cha mwisho kilichofanyika Machi 2, mwaka huu, kati yao na serikali jambo la kwanza walilokubaliana ni kutengeneza mazingira mazuri ya majadiliano ikiwemo kuwaondoa Mawaziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Agenda ya pili, kwa mujibu wa Mkopi, waliyokubaliana ni kuwa baada ya mawaziri hao kujiuzulu ingefuata kujadili madai ya madaktari; na ya tatu ni kutiliana sahihi ya makubaliano ambayo wangeweza kufikia mwisho wa kikao hicho.
Aliongeza kuwa kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoitoa juzi kwa waandishi wa habari kuwa anawashangaa madaktari kwa vile suala la mawaziri halikuwa ajenda, Rais huyo wa madaktari alisema serikali imeshindwa kutekeleza agenda ya kwanza ya kujiuzulu kwa mawaziri hao na hivyo hawawezi kudandia agenda ya pili kabla ya kwanza haijapatiwa suluhu.
Daktari huyo alisema serikali inapaswa kujua kwamba mawaziri hao wawili hawawezi kuwa muhimu kama ulivyo uhai wa wananchi wa taifa hili na hawaoni sababu gani wanawang’ang’ania huku wakijua wazi kwamba ndiyo kikwazo cha kufikia suluhu ya madai yao.
Katika ushauri wake, Dk. Mkopi aliwataka mawaziri hao kujiuzulu wenyewe bila kuisubiri serikali kwa kuwa sio kweli kwamba hakuna watu wengine wanaoweza kuzishika nafasi zao.
Dk. Mkopi alifichua siri nyingine kuwa kuwa serikali imeshindwa kuanza kuwalipa nyongeza ya posho hadi sasa kama ilivyoahidi katika kikao chao cha mwisho na waziri.
Daktari huyo alisema hawaoni kama serikali ina nia njema katika kumaliza mgogoro huo na kusisitiza kwamba huenda unatatuliwa kisiasa.
Pia alielezea kuwa kitendo cha madaktari wa mkoani Dodoma kuendelea kuripoti polisi hadi sasa, wakati Waziri Mkuu wakati wa kumaliza mgomo uliopita aliahidi kwamba hakuna mtu yeyote ambaye angebughudhiwa kutokana na mgomo ule, kinatia shaka kama kweli serikali inatilia maanani suala letu.
Katika kikao cha juzi, Rais wa Chama cha Madaktari Nchini (MAT), Namala Mkopi, alisema ikiwa serikali haitawawajibisha mawaziri hao, wataanza mgomo mzito ifikapo Machi 7.
“Kama serikali iliwaonea aibu au huruma waziri na naibu wake, hatutakuwa na cha kufanya zaidi ya kurejea kwenye mgomo ambao utakuwa mkubwa zaidi ya ule uliyopita,” alisema.
Wakati huohuo mmoja wa madakatari bingwa wa magonjwa ya moyo mkoani Mbeya amemwandikia barua waziri wa afya ya kuacha kazi kwa madai kwamba haridhishwi na mazingira ya kufanyia kazi.
Daktari huyo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu nyingi za msingi.
Alisema kuwa mgogoro wa madaktari haulengi kupigania tu maslahi yao, bali wanachopambana na serikali kwa sasa ni kuona wanatengenezewa mazingira bora ya kufanyia kazi.
Alisema haiwezekani daktari kama yeye anafika wodini anakuta wagonjwa alioenda kuwatibu wamelala chini; na hakuna vifaa kama ‘gloves’.
Anasisitiza kuwa jambo hilo linamfanya awe katika wakati mgumu wa kuwapatia tiba wagonjwa.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment