RAIS Jakaya Kikwete amewaeleza madaktari kuwa, atatekeleza ahadi zake kwao lakini mgomo uliokwisha uwe wa mwisho. Amewashukuru kwa kumuamini na kurejea kazini.
Amewashangaa wanaharakati waliojitokeza katika kipindi chote cha mgomo wa madaktari na kuilaumu Serikali, badala ya kutumia nafasi zao kutetea uhai wa Watanzania wao walikuwa wanaunga mkono mgomo.
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam jana, aliwataka madaktari hao kumuamini na
kumwachia kazi ya kushughulikia madai yao na kusisitiza kuwa mgomo huo usijirudie na badala yake taaluma na Sheria za nchi vizingatiwe.
“Nawashukuru madaktari kwa kuniamini na kurejea kazini, lakini pia nawaomba waniamini, ninawahakikishia kuwa tunawathamini na kuwajali na tutafanya yale yote yaliyo chini ya uwezo wetu, yatakayotushinda hatuwezi kuwaahidi ila tutajitahidi,”alisema Rais Kikwete.
Alisema katika nchi nyingine sheria zao ni kali zaidi kwani iwapo daktari atasababisha kifo cha mgonjwa kwa kugoma, hushitakiwa kwa tuhuma za kuua bila kukusudia.
“Sheria hii kwetu ipo lakini haina masharti haya wala hatutarajii kuyaweka.” Aliwataka madaktari kutambua kuwa kazi yao haifanani na kazi nyingine, kwani wanapogoma waathirika wakubwa huwa ni wananchi ambao hupoteza maisha.
“Dereva wa daladala akigoma athari ni watu kutembea kwa miguu lakini si kupoteza maisha, nawaomba huu uwe mgomo wa mwisho zingatieni taaluma yenu na sheria za nchi.”
Hata hivyo, alisema pamoja na juhudi zote hizo madaktari hao walikutanishwa na maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na ndipo walipokutana na Rais Kikwete na kufikia makubaliano ya kuendelea na mazungumzo huku wakiwa wamerejea kazini.
Rais Kikwete aliahidi kutowaangusha madaktari hao kwani tayari suala lao la nyongeza ya posho limepitishwa na kinachosubiriwa ni majibu kutoka Hazina, lakini pia aliwasisitiza wakati mazungumzo yakiendelea waepuke kuipa Serikali masharti kwa kuwa siku zote wanaozungumza hawagombani.
Kuhusu mawaziri alisema jambo la msingi si kuwasimamisha viongozi hao ila ni kuhakikisha mambo ya msingi yanafanyiwa kazi, kwa kuwa mawaziri ni viongozi wa kisiasa, ambao hupita tu katika wizara.
Alisema, pamoja na kwamba mgomo huo umekwisha na suala hilo kuendelea kushughulikiwa, amejifunza kuwa kuna tatizo kubwa la pande mbili kutoamiana, hali iliyosababisha kutokea kwa mgomo huo ulioleta maafa kwa watu wasio na hatia.
“Jambo la kusikitisha katika mgomo huu wapo wengine walioingilia, si mnajua adui yako mwombee njaa, wanaharakati walisimama na kuzungumza mengi, sawa tunayapokea, lakini kama wao ni watetea haki za binadamu hivi jamani kuna haki kubwa zaidi ya maisha ya watu?” Alihoji.
No comments:
Post a Comment