![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEirk6JUl6n9scrPnixx3VkrmE5fZDsVzJCAzCto2sjdUsp6nWTEuN5FxVzjxU696OM5POKBZZEXGHjW6Itma3JASjqX1xD76HaJDlbpDkew91YSwVI3TYDSX2vK0dBzcME6omEoIJoq1mg/s320/mdee.jpg)
Akiwahutubia mamia ya wananchi katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika Jimbo la Arumeru Mashariki jana, Mdee alisema kuwa Lowassa anataka kuwaghilibu Watanzania kuwa anaumizwa na tatizo la ukosefu wa ajira wakati akijua ni matokeo ya kushindwa kwa sera na mipango ya chama na serikali yake, ambayo yeye mwenyewe amekuwa sehemu ya uongozi wake kwa muda mrefu.
Akiwa katika Kijiji cha Ndatu katika Kata ya Poli, Mdee aliwaambia wananchi kuwa kama Lowassa ana uchungu na vijana na nchi hii kwa ujumla, alipaswa kuwa ameonesha hilo kwa kutoa ushauri anaoutoa sasa wakati akiwa madarakani, na si wakati huu ambapo amekuwa akiandamwa na tuhuma za ufisadi hata ndani ya chama chake.
Mdee aliongeza kuwa kama kweli Lowassa, ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu Februari 2008 kwa kashfa ya ufisadi wa kampuni tata ya Richmond, hataki nchi ilipuke, basi akishauri chama na serikali yake kuziba mianya yote ya ufisadi na kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wote wa ufisadi nchini ambao wametumia nafasi zao kuwaibia Watanzania na kuifilisi nchi.
Mbunge huyo alisema kuwa Lowassa anawadanganya wananchi akionesha kuwa ana uchungu na tatizo la ajira kwa vijana, bali ana matamanio ya urais, kwa kuwa alikuwa serikalini na ndani ya chama chake kwa muda wote huo, na wala tatizo la ukosefu wa ajira halikuanza leo wala halikuchipuka kama uyoga.
“Hili limesababishwa na kushindwa kwa mfumo, sera na mipango ya chama kilichoko madarakani sasa lakini pia mafisadi wamesababisha vijana kukosa ajira, hivyo ufisadi ndio tishio kubwa kabisa kwa nchi kwa sasa.
“Namwambia Lowassa kabla tatizo la ajira kwa vijana halijafikia kilele cha kulipua nchi, ufisadi unaofanywa na viongozi wa CCM na serikali utakuwa umeshailipua nchi hii, hivyo azungumzie ufisadi kwanza…tena asiende mbali, apekue tu nyaraka za CHADEMA aangalie tamko letu la Mwembeyanga mwaka 2007, ambapo tulitaja orodha ya aibu ya mafisadi na ufisadi ndipo apige kelele,” alisema Mdee.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment