Tuesday, March 13, 2012

CCM yatikisa Arumeru

MJI wa Usa River katika Wilaya ya Meru jana ulitikiswa na kishindo cha uzinduzi wa kampeni za CCM, ulioongozwa na Mwenyekiti wake Mstaafu, Benjamin Mkapa.


Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ngaresero, Mkapa alikanusha kuwa na ubia na kampuni ambazo zimewekeza katika maeneo makubwa ya ardhi ya Meru.


Suala la migogoro ya ardhi ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wa wilaya hii na jana Mkapa alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kukanusha kwamba ana ubia na wale aliowaita kuwa ni walowezi katika wilaya hiyo.


“Kwanza kabisa nataka niweke mambo sawa, nimesikia kwamba ninahusishwa na hawa wamiliki wa ardhi, eti kina nani hawa… ndiyo Jerome sijui Jerome, huu ni uzushi na hauna ukweli wowote,” alisema Mkapa alipokuwa akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari na kuongeza:


“Mimi katika nchi hii sijawahi kumpokonya mwananchi yeyote shamba, wala kumnyanyasa Mtanzania yeyote kwa kumpokonya ardhi, nimekuwa mtetezi wa kuhakikisha kila watu wanapata haki ya matumizi yao ya ardhi, haya maneno mengine ni uzushi na upuuzi wa hali ya juu.”


Alisema amepokea taarifa za kuwapo kwa migogoro mikubwa ya ardhi inayosababishwa na baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa na kusema atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kumshauri achukue hatua kwa kuwawajibisha watendaji wa Serikali ambao wameshindwa kuwajibika na kuchukua hatua kwa wawekezaji waliokiuka masharti.


“Yapo matatizo kadha wa kadha, wapo wawekezaji ambao wamehodhi maeneo makubwa wakati hawayatumii, wapo ambao wamechukua maeneo na kubadilisha matumizi yake na wapo ambao wamekiuka sheria za uendeshaji wa maeneo waliyopewa,” alisema Mkapa na kuongeza:


“Yote haya nimeyapokea na nitayafikisha kwa Mwenyekiti wangu wa CCM ambaye pia ni Rais wangu ili ayashughulikie baada ya uchaguzi maana tukifanya sasa, hawa wenzetu (wapinzani) watasema tumewahonga wananchi.”


Aidha, Mkapa alikanusha taarifa kwamba alitoa masharti baada ya kuombwa kuongoza uzinduzi wa kampeni hizo za CCM:


“Mimi ninamheshimu sana Mwenyekiti wangu wa CCM na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama maana nimezaliwa CCM na kukulia ndani ya CCM. Kwa maana hiyo siwezi hata siku moja kuhoji au kutoa masharti pale ninapoombwa na chama kutekeleza jukumu lolote.”


ShamrashamraShamrashamra za CCM zilianza asubuhi kwa magari na pikipiki zilizopambwa kwa bendera za kijani na njano kupita katika mitaa mbalimbali ya Usa River, zikiwahamasisha wakazi wa mji huo kuhudhuria uzinduzi huo.


Mapema viongozi kadhaa wa chama hicho walitawanyika katika kata zote 17 za Arumeru Mashariki kulifanya mikutano ya ndani kwa lengo la kuwaweka sawa makada wao ambao wanadaiwa kuchanganywa na taarifa kwamba chama hicho kimegawanyika kuhusu mgombea wao, Sioi Sumari.


Baadaye mchana, msafara wa mgombea huyo wa CCM ulianza kuelekea katika eneo la mkutano ukitokea katika Hoteli ya Gateway ukisindikizwa kwa magari na pikipiki.


Kabla ya msafara huo kuondoka, kulikuwa na kikao cha ndani kilichofanyika hotelini hapo kikiwahusisha viongozi wa chama hicho na taarifa za ndani zinadai kwamba kilikuwa kikipanga mikakati ya mkutano huo wa uzinduzi.


Msafara huo ulitoka hotelini hapo saa 9.15 alasiri na kuingia Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, njia ya Leganga na kuelekea moja kwa moja katika Ngarasero.


Wakati msafara huo ukiwa Barabara ya Leganga ukielekea uwanjani, ulipita karibu na kambi waliyofikia viongozi mbalimbali wa Chadema na baadhi ya makada wa chama hicho walijitokeza na kuzomea msafara huo.


Msafara huo uliwasili uwanjani hapo robo saa baadaye na viongozi wake waliungana na wanachama wao waliokuwa uwanjani hapo tayari kwa uzinduzi.


Chanzo:Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment