Saturday, February 18, 2012

Waziri Sitta matatani

WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ameingia matatani baada ya Jeshi la Polisi nchini kutolea tamko ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe na kueleza kuwa hautokani na kulishwa sumu, huku likisema limefungua jalada kwa ajili ya uchunguzi wa kauli yake hiyo.


Tamko hilo la polisi lililotolewa jana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. DCI Manumba aliwataka watu kuupuza madai hayo akieleza kuwa ushahidi uliopatikana kutoka nchini India alikolazwa Dk Mwakyembe hauonyeshi kuwa alilishwa sumu.


Manumba alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari jijini Dar es salaam muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake kuhusu hali na mwenendo wa uhalifu nchini katika kipindi cha mwaka jana.


Akifafanua kuhusu kauli hiyo ya Waziri Sitta, DCI Manumba alisema, "Jeshi la Polisi limekaa kimya muda mrefu likifanyia uchunguzi kauli hiyo kwa kuwa maneno hayo ndani yake yanaonyesha jinai."


Aliendelea “Kazi ya Jeshi la Polisi ni kuchunguza makosa na si kufuatilia nani anaumwa ugonjwa gani. Nani anaumwa nini ni jukumu la madaktari. Lakini tumekuwa kimya muda mrefu tukichunguza tuhuma hizo nzito.’’ DCI Manumba aliendelea kufafanua “Ukweli kuhusu kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya ambayo nayo imewasiliana na hospitali aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa zinaonyesha kuwa hakuna sumu katika maradhi yanayomsibu Mwakyembe.’’


Manumba aliongeza kuwa kwa kuwa suala hilo ni la kisheria na kiupelelezi, Jeshi la Polisi linaandaa jalada la upelelezi kuhusu kauli hiyo ya Waziri Sitta na likikamilika, litapelekwa kwa DPP kwa ajili ya uamuzi.


“Hata hivyo, Sitta mwenyewe nilimsikia katika kauli yake akisema kuwa naye ameisikia katika vyombo vya dola, hivyo tunaandaa jalada la upelelezi na likikamilika litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kwa uamuazi wa kisheria wa nani ashitakiwe au nani ana makosa. Lakini sasa ni hayo kuhusu kauli hiyo Waziri Sitta ninayoweza kusema,’’ alisema Manumba.


Awali Manumba alisema kabla Dk Mwakyembe hajaanza kuumwa na kukimbizwa India kwa matibabu, Jeshi la Polisi lilipokea maandishi kutoka kwa waziri huyo yaliyodai kuwa alikuwa akitishiwa uhai wake, lakini likiwa katika hatua za mwisho kukamilisha upelelezi wake, akaanza kuugua na kukimbizwa India kwa matibabu.


“Jeshi la Polisi liliwahi kupata maandishi kutoka kwa Mwakyembe kuwa anatishiwa uhai wake, lakini tukiwa katika hatua za mwisho za uchunguzi, Mwakyembe akaanza kuumwa,’’ alisema Manumba.


Historia ya ugonjwa wa Mwakyembe Dk Mwakymbe alianza kuumwa Oktoba 9 mwaka jana na baadaye kupelekwa nchini India na kulazwa katika Hospitali ya Apollo kwa matatibu.


Alirejea nchini Desemba 11, mwaka jana baada ya kulazwa hospitalini humo kwa takribani miezi miwili. Msemaji wa familia ya Dk Mwekyembe na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa alisema mara baada ya mbunge huyo wa Kyela kurudi nchini kuwa, afya yake ni nzuri ndio maana ameruhusiwa kutoka hospitali. Kauli za Waziri Sitta


Mara kadhaa Waziri Sitta amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa ugonjwa wa Dk Mwakyembe, umetokana na kulishwa sumu. Akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Jijini Dar es Salaam Januari 28 mwaka huu, Sitta alisema:“


Nasema Dk Mwakyembe kapewa sumu, kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka,” alisisitiza Waziri Sitta katika hafla hiyo.


Sitta alihoji “ Ni vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia, lakini baada ya saa moja unarudia tena, kitu hicho si cha kawaida.”


Sitta alisema wamejaribu wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment