Wednesday, February 15, 2012

Mwakyembe kurudi India kutibiwa

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe anatarajia kuondoka nchini wakati wowote kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.


Dk Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9 mwaka jana, alilazimika kupelekwa katika Hospitali ya Appolo nchini India kwa matibabu zaidi.


Jana, vyanzo vya karibu na Dk Mwakyembe vilidokeza gazeti hili kwamba naibu Waziri huyo na Mbunge wa Kyela anatarajiwa kurudi Appolo, kwa ajili ya kuangalia kama matibabu aliyopata yameweza kumsaidia kwa kiwango gani.


Vyanzo hivyo vilivyo karibu na Dk Mwakyembe, vilifafanua kwamba anachokwenda kufanya India ni "Uchunguzi tu wa kawaida kuona maendeleo ya matibabu."


"Atarudi katika uangalizi wa kawaida, kwasababu amekuwa akipata matibabu hivyo lazima achunguzwe kuona dawa alizokuwa akitumia zimemsaidia kwa kiwango gani," alisema.


Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, hivi karibuni alijitokeza na kutoa kauli nzito kuhusu chanzo cha maradhi yanayomsibu, huku Serikali ikiendelea kukaa kimya hata baada ya washirika wake wa karibu kusisitiza kwamba alipewa sumu.


Itakumbukwa kwamba, mwaka jana, Dk Mwakyembe akiwa na hali mbaya alipelekwa katika Hospitali ya Appolo, nchini India kwa matibabu baada ya kuugua maradhi yaliyosababisha ngozi yake kuharibika.


Tangu arejee mwanzoni mwa mwezi uliopita alikuwa hajaonekana hadharani, mbali na kutoa tamko kwamba afya yake ilikuwa inaendelea vizuri.


Hata hivyo, muda wote huo aliokuwa nchini India na baada ya kurudi nchini, mazungumzo ya watu maofisini, nyumbani, mitaani na vijiweni yalitawaliwa na utata wa suala la afya ya Dk Mwakyembe, huku uvumi, tetesi na minong’ono kwamba maradhi yake yalisababishwa na hujuma za kisiasa vikitawala hisia za wananchi.


Hisia hizo zilikuzwa na kauli ya mmoja wa washirika wake kisiasa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta ambaye alimtembelea hospitalini nchini India na baadaye kutoboa hadharani kwamba Dk Mwakyembe alikuwa amelishwa sumu kutokana na msimamo wake dhidi ya mafisadi.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment