MJI wa Songea na viunga vyake jana ulikumbwa na machafuko makubwa yaliyofanya polisi waue watu wanne baada ya wananchi kuandamana wakipinga mauaji yanayodaiwa kuambatana na imani za kishirikina tangu Novemba mwaka jana.
Katika machafuko hayo watu wengine 41 walijeruhiwa, wawili wakiwa katika hali mbaya huku shughuli za kiuchumi na kijamii zikisimama kwa muda.
Hata hivyo, idadi hiyo ya vifo na majeruhi inatofautiana kati ya ile iliyotolewa na jeshi la polisi, uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Wakati polisi ikisema waliokufa ni wawili na majeruhi ni 10, uongozi wa hospitali ya mkoa umesema umepokea maiti nne na majeruhi 41 na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inasema waliokufa ni wawili na majeruhi ni 20.
Tukio hilo la kwanza kutokea katika historia ya Mji wa Songea, lilitokana na hatua ya wananchi kuamua kuandamana kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuelezea kilio chao baada ya kuwepo kwa mauaji ya mara kwa mara ya raia tangu Novemba mwaka jana ambao baada ya kuuawa wamekuwa wakinyofolewa sehemu zao za siri.
Hadi jana, imeripotiwa kwamba watu tisa wameshapoteza maisha katika mazingira hayo kwa nyakati tofauti.
Habari zilizopatikana mjini Songea zinasema kwamba mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kishirikina yakidaiwa kufanywa na wachimba madini wa migodi iliyoko nchi jirani.
Maandamano na vuruguMaandamano hayo yaliibuka baada ya jana asubuhi mtu mmoja wa kiume kukutwa amekufa kwa kukatwa mapanga eneo la Makarawe huku pia sehemu zake za siri zikiwa zimenyofolewa.
Baada ya kuuona mwili huo wa marehemu, umati wa watu ulianza kukusanyika na kuamua kuandamana wakisema kwa amani ili kuwasilisha kilio chao kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Maandamano hayo yalivuta umati watu na mamia ya wananchi walijiunga na kuanza kutembea kwa miguu huku wengine wakiwa katika pikipiki maarufu kwa jina la 'Yeboyebo,' kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zilizo jirani na Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Ruvuma.
Kadri wananchi hao walivyokuwa wakiendelea kuandamana, habari zilitapakaa mitaa mbalimbali na kuwafanya wananchi wengi zaidi kuungana nao, hali iliyowalazimu polisi nao kujipanga kuwazuia kwa kutumia mabomu ya mchozi.
Hata hivyo, wananchi walizidi kuongezeka wakipinga hatua hiyo ya polisi kuwazuia kufikisha ujumbe wao kwa Mkuu wa Mkoa.
Katika hatua hiyo, ndipo vurugu zilipoanza kwani wakati polisi watumia mabomu ya kutoa machozi, baadhi ya waandamanaji walianza kuvurumisha mawe hali iliyowafanya watu kukimbia huku na huko.
Vurugu zilishika kasi hali iliyowafanya polisi kuanza kutumia risasi za moto katika kile ilichodai baadaye kwamba ni katika kujilinda na ndipo vifo hivyo vilipotokea na idadi hiyo kubwa ya majeruhi.
Hata hivyo, haikuelezwa mara moja kama miongoni mwa majeruhi hao alikuwamo askari polisi.
Baada ya mauaji hayo, vurugu zilizidi kusambaa katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Songea huku wananchi wakianza kurusha mawe kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi.
Lakini wengine waliendelea kupigia kelele madai yao ya msingi huku wakilishutumu jeshi hilo kwa kushindwa kudhibiti mauaji hayo kwa muda mrefu.
Vurugu hizo zilisababisha ofisi za Serikali na taasisi binafsi mkoani Ruvuma kufungwa kwa muda yakiwemo maduka, masoko na huduma za kifedha katika mabenki kusimama kwa muda.
Huduma za usafiri katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani nazo zilisimama, huku madereva wa mabasi na abiria wakikimbia kujificha kuepuka mabomu ya machozi na risasi za moto zilizokuwa zikipigwa hewani.
Pia huduma za matibabu katika Hospitali ya Mkoa zilisimama kwa muda baada ya walinzi wa hospitali hiyo kufunga lango kuu, kutokana na wananchi wengi kukimbilia huko wakikimbia mabomu.
Habari zaidi kutoka eneo la tukio zimeeleza kuwa maandamano hayo yalichochewa na taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa juzi kwamba mauaji hayo yanahusiana na masuala ya kipenzi.
Ilielezwa kwamba wananchi walikuja juu wakipinga madai hayo ambayo pia yaliripotiwa jana na gazeti hili.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment