Tuesday, February 21, 2012

'Kikwete toa kauli ugonjwa wa Mwakyembe'

RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kutoa kauli dhidi ya ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, baada ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, kutoa kauli zinazopingana.


Sambamba na hilo, kiongozi huyo wa nchi amebebeshwa mzigo wa Dk. Mwakyembe, kwa madai kuwa ugonjwa uliompata ni matokeo ya Serikali ya Rais Kikwete kushindwa kuwashughulikia mafisadi waliotajwa na Dk. Mwakyembe katika ripoti ya uchunguzi kuhusu sakata la zabuni ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.


Akizungumza na gazeti hili jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashir Ally, alisema ukiachia suala la viongozi waandamizi kutoa kauli za kupingana, chanzo cha ugonjwa wa Dk. Mwakyembe ni serikali kushindwa kuukabili ufisadi.


“Ukiweka kando suala la viongozi kutoa kauli za kujikanganya kuhusu ugonjwa wa Mwakyembe kwamba amelishwa sumu au la, lakini ukiliangalia jambo hili utabaini kuwa chanzo chake ni ufisadi, na niseme kwamba hatua hii, mafisadi wameteka dola na hii ni hatari sana kwa taifa,” amesema.


Amesisitiza kuwa mafisadi wameteka dola kwani hata waliohusika na wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), wapo mitaani wakiendelea kuishi na wale walioibua ufisadi huo, hali ambayo ni hatari.


Akizungumza kwa kujiamini, Dk. Bashir amesema kama serikali ya Rais Kikwete ingetekeleza mapendekezo ya ripoti ya Dk. Mwakyembe, leo hii hofu kwamba kalishwa sumu, isingekuwepo na ugonjwa wake ungeonekana wa kawaida.


Akizungumzia suala la viongozi kutoa kauli za kujikanganya katika mambo muhimu yanayolihusu taifa, Dk. Bashir amesema hiyo ni aibu, kwani si mara ya kwanza kwa viongozi wa serikali kupishana kwenye kauli zinazohusu mambo muhimu ya taifa.


Aliitaka serikali kukata mzizi wa fitina kwa kutoa kauli sahihi kuhusu ugonjwa wa Dk. Mwakyembe ili wananchi wajue ukweli.


Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake nchini (TAMWA), Ananilea Nkya, amesema ni aibu kwa serikali kuwa na kauli za kujikanganya kuhusu afya ya naibu waziri huyo.

Amesema hali hiyo si tu kwamba ni aibu bali pia inaonyesha serikali inataka kucheza na afya ya kiongozi huyo.


“Serikali imewaweka wananchi njia panda kuhusu afya ya Dk. Mwakyembe, hawajui washike lipi, Waziri Mkuu anasema lake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, naye katoa kauli tofauti na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Manumba, hapa wananchi washike lipi?” alihoji Nkya.


Mkurugenzi huyo wa Tamwa alisema, kwa hatua iliyofikiwa ni bora Rais Kikwete akazungumzia tukio hilo ili kurejesha imani kwa wananchi, vinginevyo watabaki njia panda, wasijue wamwamini nani.


Alisisitiza kuwa suala la ugonjwa wa kiongozi yeyote haliwezi kuwa siri kiasi cha serikali kushindwa kuzungumzia, kwani siku zote viongozi huenda kutibiwa nje kwa gharama za kodi za wananchi.


Katika hatua nyingine, baadhi ya askari polisi wameelezwa kushangazwa kwao na kauli ya bosi wao, Manumba.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, huku wakiomba majina yao yahifadhiwe, askari hao walisema DCI Manumba asingezungumzia kabisa suala hilo kwani bado liko kwenye uchunguzi.


“Wiki takriban mbili zimepita tangu Waziri wa Mambo ya Ndani aliposema serikali imeamua kuchunguza sakata hili. Kwa vyovyote vile uchunguzi unaendelea, yeye taarifa kwamba uchunguzi umekamilika na Mwakyembe hajalishwa sumu ameipata wapi?” alihoji askari mmoja wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini.


Juzi Manumba alikaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba uchunguzi wa ugonjwa wa Mwakyembe umekamilika na kwamba hajalishwa sumu.


Kauli hiyo ilimuibua Dk. Mwakyembe ambaye kupitia taarifa yake alisema haamini kama taarifa aliyosoma DCI Manumba ni yake, kwani haikuwa sahihi na imejaa upotoshaji.


Taarifa za Dk. Mwakyembe kulishwa sumu mara ya kwanza ziliibuliwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta.


Ugonjwa huo umesababisha kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, anyonyoke nywele, kope, vinyweleo na ndevu, huku vidole vya mikono na kucha zake zikiwa nyeusi, hali inayomfanya avae ‘gloves’ muda wote.


Halikadhalika miguu ya Dk. Mwakyembe ambaye kwa sasa amerejea nchini India kwa matibabu imevimba na kupasuka na wakati mwingine hutoa damu, hali inayomsababishia maumivu makali.


Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment