Tuesday, January 24, 2012

Cheti cha Form 6 chasababisha Polisi aue ndugu zake 2

MAUAJI ya watu wawili yaliyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi, kituo cha Magomeni Dar es Salaam, Nicodemus Senge, chanzo chake kinadaiwa kutokana na mmojawapo kufanikiwa kimaisha kwa kutumia cheti cha mwenzake cha kidato cha sita.


Anayedaiwa kufanikiwa kimaisha ni Nicodemus Senge ambaye alikuwa mtumishi wa Bunge, kitengo cha Ununuzi na Ugavi. Mwingine aliyeuawa katika tukio hilo ni Andrew Nkollo.


Chanzo cha habari, kililiambia gazeti hili jana kuwa pamoja na kuwapo ugomvi wa shamba walilokuwa wakigombea, lakini hali ilibadilika zaidi kutokana na ofisa huyo wa Bunge kuonesha kiburi cha fedha na hata kumtolea maneno ya kejeli nduguye.


Katika ugomvi huo, Nicodemus wa Bunge anadaiwa kutumia cheti cha Inspekta huyo wa Polisi na jina lake.


Miili ya marehemu hao iliagwa jana katika sehemu mbili tofauti, ambapo miili ya Nicodemus wa Bunge na Andrew iliagwa kwa pamoja katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lililopo Hospitali ya Taifa Muhimbili na kusafirishwa kwenda Arusha kwa maziko, wakati mwili wa Nicodemus wa Polisi uliagiwa nyumbani kwake katika kota za Polisi Msimbazi na kusafirishwa kwenda Singida kwa maziko.


Ilidaiwa kuwa hata familia za marehemu hao zilikuwa hazielewani na mara kwa mara zilizodoana, hadi kufikia wakati kutoleana maneno ya kukashifiana kuwa wanaringa wakati fedha walizonazo zinatokana na kutumia cheti cha Nicodemus wa Polisi.


Aidha, chanzo hicho kilifafanua kuwa ni kweli kuna shamba la ekari mbili lililoko Iramba mkoani Singida ambalo linadaiwa kumilikiwa na Andrew ambaye ni mtoto wa shangazi yao akina Nicodemus na ugomvi wa wawili hao ulianza pale Nicodemus wa Polisi alipomjengea nyumba mama yake mzazi katika shamba hilo ambapo alitakiwa atoe fedha ili aachiwe eneo hilo.


Hata hivyo, ilielezwa kuwa wakati wawili hao wakigombana, Andrew alikuwa akipewa nguvu na Nicodemus wa Bunge ili Nicodemus wa Polisi ikiwezekana aiondoe nyumba hiyo eneo hilo.


Pia ilidaiwa kuwa ugomvi huo ulifika mahakamani lakini ufumbuzi haukupatikana hivyo kuamua kukaa ili kupata suluhu na kikao kufanyika nyumbani kwa baba mdogo wao, Pendael Senge anayeishi Kongowe, Kibaha.


Katika kikao hicho, inadaiwa Nicodemus wa Bunge alisimama na kumtolea maneno ya jeuri polisi huyo, kwamba kikao hicho alikidhamini kwa fedha kwa wajumbe ndipo mtafaruku ulipoanza ambapo Inspekta alisimama na kumpiga risasi ofisa huyo wa Bunge kichwani na kumwua pale pale.


Mbali na kumuua ofisa huyo wa Bunge, pia Nicodemus wa Polisi alimuua binamu yake kwa kumpiga risasi mbili za kifuani na yeye mwenyewe kujipiga risasi kifuani karibu na moyo wake.


Chanzo: Gazeti la Habarileo

No comments:

Post a Comment