Wednesday, August 3, 2011

Japan- Samaki walioingizwa Tanzania hawana mionzi

Mlipuko baada ya tsunami nchini Japan
Waathirika wa janga la Tsunami nchini Japan

Ubalozi wa Japan nchini Tanzania umesema, samaki walioingizwa Tanzania hawana mionzi.


Samaki hao aina ya bangala (mackerel) waliingizwa Tanzania kutoka Japan.


Kwa mujibu wa ubalozi huo, hawana aina yoyote ya mionzi inayoweza kusababisha madhara kwa binadamu.

Taarifa iliyotolewa na Ubalozi huo imesema, tani 124.992 za samaki hao zilifanyiwa ukaguzi na shirika la ukaguzi wa vyakula vinavyoharibika, Japan Frozen Foods Inspection Corporation (JFFIC), lililoko Yokohama na kubainika kutokuwa na mionzi hiyo.


Hofu ya mionzi hiyo inatokana na tetemeko la ardhi lililotokea nchini humo Machi 11 Fukushima na kusababisha uharibifu mkubwa wa kinu cha nyuklia chenye kutoa mionzi hatari.


“Baada ya tukio la tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 11 Machi, 2011, Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Kilimo, Misitu na Uvuvi za Japan zimekuwa zikifanya ukaguzi wa mara kwa mara wa maji na chakula, ili kubaini kama kuna dalili za mionzi hatari,” ilisema taarifa hiyo.


“Katika uchunguzi huo hapajaonekana athari zozote katika mazao ya baharini hususani samaki aina ya bangala. Kama samaki hawa walivuliwa kabla ya tarehe 11 Machi 2011, hakuna uwezekano kuwa wameathirika na mionzi ya nyuklia,” ilisema taarifa.



Samaki hao walivuliwa katika mwambao wa Choshi, ulioko Chiba Desemba 16 na 17 mwaka jana na kusafirishwa hadi bandari ya Hasaki iliyopo Ibaraki, Desemba 17 mwaka huo huo. “Kwa msingi huo samaki hawakuathirika na mionzi ya nyuklia.


“Tunapenda kuhitimisha kuwa hawa samaki wa bangala kutoka Japan wamezoeleka Tanzania kutokana na urahisi wa kupatikana na wana lishe nzuri. Pia wamekuwa chanzo cha protini kwa walaji, hivyo ni imani yetu kuwa ulaji wa samaki hawa utaendelea.


“Japan ina imani pia kuwa Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi ambazo zinanunua bidhaa za chakula kutoka Japan na hatua zaidi zinachukuliwa kuongeza ushirikiano kati ya nchi zetu mbili,” ilihitimisha taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment