Friday, July 22, 2011

Jairo yupo likizo, anachunguzwa

David Jairo
Barua iliyomponza Jairo

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, amepewa likizo kuanzia leo ili Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali amchunguze.

Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, alisema jana mjini Dodoma kwamba, tuhuma zinazomhusu Jairo ni za fedha, na kwamba, CAG kapewa siku 10 achunguze Jairo.

Luhanjo amesema, ndani ya siku kati ya mbili na tatu, atakuwa amemteua mtu wa kukaimu nafasi ya Jairo.


Amesema, wakati Jairo akiwa likizo hiyo ya lazima atalipwa mshahara kama kawaida.

Luhanjo amesema, tuhuma dhidi ya Jairo ni nzito na imemlazimu kuamua aende likizo licha ya kwamba Sheria namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za utumishi wa umma za mwaka 2003, inaruhusu mtuhumiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi ukifanywa.

Amesema, tuhuma zinazochunguzwa ni zilizotolewa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini.

Jairo anatuhumiwa kuzitaka taasisi, vitengo na idara zilizo chini ya wizara hiyo, zichangie Sh milioni 50 kila moja, ili fedha hizo zitumike kulipa wabunge na kufanikisha mawasilisho ya makadirio hayo.

Tuhuma zingine ni za kulipa masurufu ya safari watumishi walio chini ya wizara hiyo na taasisi zake, ambao tayari walishalipwa na wizara na taasisi hizo.

“Hataendelea na kazi kipindi cha uchunguzi. Hatua zaidi zitategemea uchunguzi huo wa awali… nimeamua niseme, msianze kubashiri, kwamba tunamsubiri Rais aliyemteua, mimi ndiye mwenye mamlaka … nikipata taarifa ya uchunguzi wa awali, nitampa notisi ya matokeo ya awali,” Luhanjo aliwaambia waandishi wa habari.

Luhanjo alisema kulingana na Sheria namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za utumishi wa umma za mwaka 2003, mwenye mamlaka ya nidhamu kwa mtumishi yeyote wa umma anayeteuliwa na Rais kasoro wanasiasa, mawaziri na wakuu wa mikoa, ni Katibu Mkuu Kiongozi.

Alisema katika kushughulikia tuhuma zinazomkabili mtumishi wa umma, lazima uchunguzi wa awali ufanyike kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma, ili kubaini kama mtumishi husika ametenda kosa la kinidhamu.


“Katika kipindi cha uchunguzi, mtumishi anayetuhumiwa, anaweza kupewa likizo ya malipo ili kupisha shughuli za uchunguzi au akaruhusiwa kuendelea na kazi wakati uchunguzi ukifanywa,” alisema Luhanjo.

Alifafanua kwamba kama uchunguzi wa awali dhidi ya Jairo, utabaini makosa ya kinidhamu, Mamlaka ya Nidhamu itampa taarifa za tuhuma ambazo zitaambatana na hati ya mashitaka, itakayoelezea kwa ufupi kosa alilotenda na ni lini anapaswa awe amejibu tuhuma husika.

Mtuhumiwa anapaswa asimamishwe kazi na kulipwa nusu mshahara.

“Mtuhumiwa atatoa maelezo yake kwa mujibu wa hati ya mashitaka aliyopewa. Anaweza kukataa au kukubali. Akikubali, Mamlaka ya Nidhamu itaendelea kutoa adhabu kulingana na uzito wa kosa. Adhabu inaweza kuwa kufukuzwa kazi, kupunguzwa cheo au kupunguzwa mshahara ama adhabu nyingine iliyoelekezwa na Sheria ya Utumishi wa Umma.

“Iwapo atakana mashitaka, Mamlaka ya Nidhamu itaunda Kamati ya Uchunguzi itakayopewa hadidu za rejea ambazo pamoja na mambo mengine, zitaeleza muda wa uchunguzi huo
kukamilika. Taarifa ya Kamati itawasilishwa kwa Mamlaka hiyo, ikiwa na mapendekezo. Ikumbukwe kuwa Kamati hii haitoi adhabu kwa mtuhumiwa isipokuwa inatoa mapendekezo tu,” Luhanjo alisisitiza.

Baada ya taarifa ya Kamati ya Uchunguzi, Luhanjo alisema Mamlaka itaendelea kutoa adhabu kwa mujibu wa mapendekezo ya Kamati hiyo. Kama adhabu itakuwa ni kuvuliwa madaraka, Mamlaka ya Nidhamu itawasiliana na Mamlaka ya Uteuzi kuhusu kutekeleza suala hilo.

Hata hivyo, Luhanjo alisema iwapo mtuhumiwa hajaridhika na uamuzi unaoishia kwa Mamlaka ya Nidhamu, sheria zinampa fursa ya kukata rufaa kwa Rais. “Rais ana mamlaka ya kuthibitisha au kukataa uamuzi wa Mamlaka ya Nidhamu,” alisema.

Tuhuma dhidi ya Jairo ziliibuliwa Julai 18 bungeni na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM).

No comments:

Post a Comment