Tuesday, May 18, 2010

Aliyeaga anakwenda misa ya kwanza afumaniwa gesti

MJI wa Moshi na vitongoji vyake, jana ulizizima baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa amemuaga mumewe kuwa anakwenda misa ya kwanza kanisa la Kristo Mfalme, Moshi,kufumwa akitoka kufanya mapenzi na kijana mmoja mbeba mizigo.

Tukio hilo ambalo lilivuta hisia za wananchi wengi ambao walifurika kituo kidogo cha polisi cha Kiborlon kushuhudia, lilitokea saa 1.00 asubuhi katika nyumba ya kulala wageni (inahifadhiwa) iliyoko eneo la Majengo mjini Moshi.

Habari zilizowakariri mashuhuda wa tukio hilo na baadhi ya maofisa wa polisi zilidai kuwa kilichomponza mwanamke huyo ni ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) aliotumiwa na hawara yake huyo akimtaka wakutane hiyo jana asubuhi.

“Jana (juzi) huyo kijana mbeba mizigo hapa Kiborlon alimtumia SMS huyo mke wa mtu, lakini kumbe mume wake aliiona na kujikausha kuwa hajaiona na ndipo leo (jana) alipotoka tu mumewe alianza kumfuatilia,” kilidai chanzo hicho.

Habari hizo zinadai kuwa baada ya mwanamke huyo kumuaga mumewe anaenda misa ya kwanza na kuondoka, mumewe alimfuatilia ambapo mke alipanda daladala maarufu kama Hiace na mumewe akakodisha Taxi.

“Mumewe aliendelea kuifuatilia hiyo Hiace kila inaposimama kwenye kituo naye anasimama kwa mbali hadi ilipofika karibu na daraja ambapo kuna kituo yule mwanamke akashuka kuelekea kwenye nyumba ya kulala wageni ,"kimefafanua chanzo hicho.

Huko ndiko mwanamke huyo mdogo kiumri alipokutana na mbeba mizigo huyo na kwenda moja kwa moja chumbani ambako mumewe baada ya kufika hapo na kuulizia alielekezwa namba ya chumba walichokuwa wameingia.

Akimkariri mume wa mwanamke huyo, polisi mmoja amesema, baada ya kuona hivyo, mume wa mwanamke huyo alirudi tena hadi eneo la Kiborlon na kuchukua vijana wengine wanne wa miraba minne.

“Walipofika pale ‘guest’ aliagiza kinywaji aina ya Konyagi na kuanza kunywa lakini walikuwa wanatazama mlango wa chumba na baada ya muda alitoka yule kijana akiwa amefuatana na mke wake,”alifafanua.

Kutokana na mshituko alioupata baada ya kumuona mumewe, mwanamke huyo alianguka ghafla na kupoteza fahamu kwa muda na alipozinduka walichukuwa pamoja na hawara yake hadi nyumba moja iliyopo Kiborloni.

Katika nyumba hiyo, mwanamme huyo alipatiwa kipigo cha nguvu kwa kutumia minyororo huku mwanamke akishuhudia na saa 2:40 waliwapeleka wote wawili kituo cha polisi, lakini mwanamme alikuwa ameumizwa vibaya.

Mwananchi mmoja wa Kiborlon aliyekuwa nje ya kituo cha polisi Kiborlon pamoja na mamia ya wananchi, Charles John maarufu kama King alisema mwanamme aliyefumaniwa alikuwa ameumizwa na alikuwa akitembea kwa shida.

Mume wa mwanamke huyo alisikika akifoka kwa hasira kituoni hapo kuwa alikuwa anataka kuachana na mwanamke huyo hapohapo kituoni, lakini polisi wakamshauri suala hilo wakalizungumze na wazazi wa pande mbili.

Baadaye polisi walimwachia mwanamke huyo ambapo alichukuliwa na mumewe na kuingizwa kwenye Taxi na mumewe alisikika akisema anamrejesha kwa wazazi wake huko Kibosho na hana mpango wa kuishi naye tena.

Mume wa mwanamke huyo ni mfanyabiashara wakati mkewe alikuwa akiuza duka la mabegi alilofunguliwa na mumewe katika eneo hilohilo la Kiborlon ambalo zamani lilikuwa ni maarufu kwa uuzaji wa nguo za mitumba.

Mnamo saa 4:30 asubuhi, 'paparazi' alishuhudia gari la kituo cha polisi Majengo aina ya Toyota Landcruiser likifika kituo cha Kiborlon na kumchukua mwanamme aliyekuwa amefumaniwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro , amesema,alikuwa hajapata taarifa hizo, lakini ofisa mmoja wa polisi alisema wameamua kuwaachia mwanamke na hawara kwa sababu fumanizi sio kosa la jinai kisheria na kwamba waliwahifadhi pale kwa muda kwa sababu za kiusalama.

No comments:

Post a Comment