Thursday, February 25, 2010

Lori lamgonga Joti, kalazwa Muhimbili

MSANII maarufu wa kundi la vichekesho la Orijino Komedi, Joti, amegongwa na gari, kalazwa katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili.

Lori la la kubeba maji linalodaiwa kuwa ni la Ubalozi wa Marekani lilimgonga Joti juzi wakati kundi hilo lilipokuwa linarekodi kipindi katika daraja la Salender, Dar es Salaam.

Muda mfupi uliopita, mmoja wa wasanii wa kundi hilo, Wakuvanga, amesema, Joti aligongwa wakati anamkimbia mlemavu omba omba aliyetaka kumpiga.

Kwa mujibu wa Wakuvanga, omba omba huyo ana mguu mmoja, na alikuwa amelewa.

Kabla ya mlemavu huyo kutaka kumshambulia Joti, alimkosa kosa mpiga picha wa kundi hilo na msanii mwingine, Mak Regan.

Amesema, wanamshukuru dereva wa lori hilo kwa kuwa alikuwa makini , alifunga breki hivyo Joti 'alipushiwa' akaanguka pembeni ya barabara.

Wakuvanga amesema, Joti aliumia kichwani, shingoni, na kisogoni.

Inadaiwa kuwa, mlemavu huyo alidhani kuwa wasanii hao walikuwa wanamrekodi yeye kwa lengo la kuwaharibia omba omba wasipate msaada.

Ajali hiyo imetokea siku chache tu baada ya kuwepo taarifa kwamba mkono wa mwanamke ulibadilika na kuwa na manyoya baada ya kumpa hela omba omba kwenye eneo hilo.

No comments:

Post a Comment