Friday, March 6, 2009

Uledi azikwa Dodoma


MWANDISHI wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communications kituo cha Dodoma, Michael Uledi amezikwa leo nyumbani kwao Buigiri, Dodoma.

Uledi aliaga dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Mirembe, Dodoma, alikuwa akiumwa kifua.

Marehemu Uledi alisoma katika shule ya msingi Buigiri 1977-1983 na baadae mwaka 1986 alijiunga katika shule ya Sekondari ya Chidya wilaya ya Masasi ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1989.

Mwaka 1990 alijiunga na shule ya sekondari ya Moshi kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita ambako alimaliza mwaka 1992 na baadae alijunga katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa mkoani Mara.

Alihitimu na kasha alikwenda Jijini Dar es Salaam ambako alifanya kazi katika kampuni binafsi kwa kipindi cha miaka miwili.

Uledi alijiunga na MAMET kwa ajili ya kozi ya Uandishi wa Habari kwa muda wa miezi mitatu na alipomaliza alijiunga na shirika la IPP mwaka 1998 ambapo alipangiwa kituo cha Dodoma akiwa ni Mwandishi wa magazeti ya Nipashe na Gadiani pamoja na Radio One.

Alijiunga na chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kilichopo mjini Dodoma mwaka 2001 hadi 2003 ambapo alimaliza Shahada ya juu ya Mipango na Maendeleo Vijijini na kufanya kazi kwa muda mfupi katika shirika la Viwanda Vidogo mkoani Dodoma (SIDO) na baadae alihamishiwa Mtwara.

Mwaka 2004 hadi 2006 alifanya kazi katika Benki ya Exims katika wilaya ya Masasi akiwa ni Meneja Msaidizi wa Bank na baadae alikaa mkoani Morogoro kwa muda mfupi ambako alikuwa akiandika katika gazeti la serikali la Habari Leo.

Januari mwaka 2007 alijiunga na kampuni ya Mwananchi Communications ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi,Citizen na Mwanasport kazi aliyoifanya hadi mauti yanamchukua.

Alikuwa ni mjumbe katika umoja wa waandishi wa habari za Bunge ambae alikuwa akiwakilisha mkoa wa Dodoma umoja ulioundwa mwaka jana.

Uledi ameacha mjane, Agnes Mzola na mtoto mmoja.

No comments:

Post a Comment