Saturday, August 8, 2009

Treni yapinduka Morogoro

Treni ya abiria iliyotoka Dar es Salaam jana kwenda Mwanza na Kigoma imepinduka usiku wa kuamkia leo mkoani Morogoro.

Treni hiyo iliyoondoka Dar es Salaam saa 11 jana jioni imepinduka katikati ya Mazimbu na Mkata, zaidi ya watu 40 wamejeruhiwa.

Ofisa Habari wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL),Midladjy Maez amesema,treni hiyo imepinduka saa nane usiku wa kuamkia leo.

Kwa mujibu wa Maez, chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika.

Amesema, kati ya majeruhi 41, saba wamejeruhiwa vibaya, na wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Morogoro.

Maez amesema, TRL imekodi mabasi 17 kuwasafirisha wasafiri ambao hawakujeruhiwa katika ajali hiyo.

Ajali hiyo imesababisha treni nyingine iliyokuwa ikitokea Bara kwenda Dar es Salaam kukwama katika eneo hilo lililoko Wilaya ya Kilosa.

Maez amesema, TRL imepeleka mabasi saba kuwasafirisha abiria waliokuwa akitoka Kigoma kwenda Dar ili wafikishwe stesheni waendelee na safari.

Amesema,kampuni hiyo pia imekodi mabasi 10 kuwasafirisha abiria waliopata ajali wanaokwenda Kigoma.
Inadaiwa kuwa watu wasiofahamika waling'oa reli muda mfupi kabla ya ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment